SAA mbili kasorobo , Mustafa baada ya
kufika ofisini , kabla ya kuanza kazi haja
ilimshika na kuelekea msalani .
Baada ya kumaliza kujisaidia alikwenda
kwenye sinki la kusafishia mikono ili
ajisafishe. Alivua pete ya ndoa na
kuiweka juu ya sinki kisha alijimwagia
sabuni ya maji mikononi na kuanza
kunawa .
Simu iliyokuwa mfukoni ilianza kuita , kwa
vile hakuweka mlio ilitetemeka kuonesha
ilikuwa inaita. Hakuipokea kwa vile bado
alikuwa na sabuni mikononi, hivyo alinawa
haraka na kufuta mikono kwa taulo dogo ili
apokee simu . Lakini kabla hajaipokea
ilikuwa tayari imekatika.
Ingawa ilikuwa imekatika lakini aliitoa ili
aangalie nani aliyekuwa akimpigia , kabla
hajaangalia simu iliita tena , kwa vile ilikuwa
mkononi aliangalia na kukuta jina la Shehna .
Japokuwa alishtuka kuona jina lile ambalo
kwake lilikuwa geni. Aliamini kuzungumza na
aliyepiga angemjua kwa vile jina lilikuwa
kwenye simu yake .
Alibonyeza kitufe cha kupokelea na kusema :
“ Haloo. ”
“ Haloo Mustafa , asalam aleiykum , ” ilikuwa
sauti ya lafudhi ya kimwambao .
“ Waleiykum msalaam, ” Mustafa aliitikia huku
akiifikiria sauti ile na kutaka kumjua
aliyempigia ambaye jina na sauti yake
vilikuwa vigeni akilini mwake .
“ Upo wapi ?” sauti ilimuuliza .
“ Nipo ofisini .”
“ Nipo ofisini kwako muda tu, lakini
mwenyeji wangu sikuoni. ”
“ Nakuja basi . ”
“ Fanya haraka kuna sehemu nawahi , nilipita
ofisini kwako mara moja . ”
Mustafa alitoka haraka kumuwahi mgeni
huyo , alimpita sekretari wake bila kumuuliza
kitu japokuwa haikuwa utaratibu mzuri
kumruhusu mgeni aingie ofisini bila
mwenyewe kuwepo . Mara zote sekretari
wake alikuwa akimruhusu mtu kuingia pale
aliporuhusiwa kufanya hivyo.
Lakini kwa kauli ya mgeni kuingia ofisini
ilionesha ameruhusiwa bila ridhaa yake .
Alipoingia ndani alishtuka alipokuta hakuna
mtu ofisini , lakini harufu ya manukato
mazuri ilisambaa kila kona .
Alitoka haraka ili amuwahi kwa kuamini
huenda aliamua kutoka baada ya kuchoka
kumsubiri. Lakini aliamini hakutumia muda
mrefu msalani .
Alikwenda hadi getini kwa mlinzi na
kumuulizia.
“ Eti kuna mgeni ametoka sasa hivi?”
“ Mgeni ! mgeni gani?” mlinzi ilionesha
kushtuka.
“ Mwanamke. ”
“ Bosi , toka uingie wewe hajaingia mtu
yeyote. ”
Popular Posts
-
“KAMA kuna watu hawayajui haya nitakayoyaongea basi nawataka kuanzia sasa wajue kwamba, hapa Dar kuna mambo makubwa sana ambayo ukisimuliwa...
-
SAA mbili kasorobo , Mustafa baada ya kufika ofisini , kabla ya kuanza kazi haja ilimshika na kuelekea msalani . Baada ya kumaliza kujisa...
Thursday, February 20, 2014
KIZAZI CHA JINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment