Popular Posts

Thursday, February 20, 2014

NYUMBA YA MAJINI

“KAMA kuna watu hawayajui haya nitakayoyaongea basi nawataka kuanzia sasa wajue kwamba, hapa Dar kuna mambo makubwa sana ambayo ukisimuliwa unaweza kusema si kweli, lakini wale wanaoyapata hayo mambo wanajua na wewe usiombe yakukute hata siku moja,” ndivyo alivyoanza kusimulia Bw. Humuli Samaki (43), mkazi wa Buguruni (kwa sasa) ambaye alipata mkasa mzito akidai alipanga nyumba moja na majini Magomeni, Dar es Salaam.
“Si zamani sana mkasa huu uliponitokea, ilikuwa mwaka 2009 tu, kwa hiyo naweza kusema ni juzijuzi.  Kwa sasa naishi hapa Buguruni, baada ya kuhama kutoka Magomeni ambako nilipataka mkasa huo mzito na wa kuogopesha. Nilipanga nyumba moja na majini.”
Awali nilikuwa nikiishi Mwanyamala Mwanjuma, jirani kabisa na Makao Makuu ya Bendi ya TOT, hata Kapteni John Komba nilizoeana naye kwa kuonanaonana pale CCM-Mwinjuma, ingawa jina langu najua hakuwa akilifahamu.
Ile nyumba niliyokuwa nikiishi Mwananyamala iliingia kwenye mgogoro wa mirathi, familia ilifika mahakamani. Hukumu ilipotoka ikaamriwa iuzwe kisha ndugu wagawane fedha.
Kwa maana hiyo, mimi na wapangaji wenzangu watano, tulipewa notisi ya kuhama baada ya mteja kupatikana. Huyu mteja anaitwa Masawe anafanya kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lakini sijui ofisi za wapi. 
Ilibidi mimi niangalie mwelekeo mwingine, niliamua nibadili upepo, nikaishi Magomeni. Kwa wakati huo nilikuwa sina familia. Sina mke wala mtoto, hata wa kusingiziwa, kwa hiyo nilikuwa naishi peke yangu. Ni mwaka jana ndiyo nimeoa mke wangu huyu.
Rafiki yangu mmoja anaitwa Mohamed Kombe alinipa namba ya dalali kwani yeye anaishi Magomeni hata sasa. Nilimpigia simu dalali wake, anaitwa Yusuf Mwamba, akaniita Magomeni pale kwenye nyumba wanayosema aliwahi kuishi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Nilikwenda mpaka pale, nilimkuta amesimama nje ya nyumba hiyo, tukasalimiana, akaniuliza nataka nyumba yenye sifa gani, nikamweleza.
Akasema nyumba ya aina hiyo ipo moja mitaa ya katikati kama unatokea pale tulipokuwa kuelekea kwa Sheikh Yahya Hussein (marehemu).
Tulikwenda kuiona hiyo nyumba. Wakati tukiwa tunaifikia, nilishangaa kuwaona majirani wakitukodolea macho, sikushangaa nikijua ni mambo ya mjini kitu kidogo tu watu kibao.
Yule dalali alifungua mlango, tukaingia ndani. Tulipita sebuleni, tukaenda kwenye vyumba viwili, tukaelekea  jikoni, chooni na kumalizia na bafuni. Ni nyumba iliyojitegemea kwa maana kwamba, ilikuwa na ua wake na mtu akiwa uani hakuna aliyeweza kuona kwa nje. Mlango wa kuingilia ndani ni mmoja tu.
Kulikuwa na vyumba vingine viwili ambavyo toka mwanzo alishaniambia kuna mtu anaishi na mkewe, kimoja wanalala, kingine wamekifanya sebuleni, lakini hawana watoto kama mimi.
Nilijiridhisha kwamba ni pazuri, dalali akaniuliza kuhusu malipo, nikamwambia tuongozane nikachukue fedha Magomeni Mapipa kwenye benki ya Barclays, akasema wakati mimi nakwenda kutoa hizo fedha, yeye anakwenda Dawasco tawi la Magomeni.
Tukiwa tunaelekea Magomeni Mapipa, nilimuuliza wenye vile vyumba wanafanya kazi wapi? Akajibu wafanyabishara, lakini hata yeye hajui ni wapi. Nilimuuliza imekuwaje ana funguo, wale wapangaji wengine wakirudi je, akajibu wana funguo yao na ile yeye alipewa na mwenye nyumba kwa ajili ya kutafutia mpangaji mwingine. Nilikubaliana naye.
***
Baada ya nusu saa nilitoka benki nikiwa na fedha, nikampigia simu, akasema na yeye alishatoka Dawasco na wakati huo alikuwa anakunywa soda kwenye Hoteli ya Shibam, ipo palepale Mapipa. Nilimfuata pale, nikampa fedha, akatoa mkataba, nikajaza kwani yeye ndiye aliyepewa jukumu lote na mwenye nyumba.
“Kwa hiyo upo huru kwenda kuhamia,” dalali aliniambia huku akinikabidhi funguo.
“Sawa, nitahamia usiku wa leo.”
Nilirudi nyumbani kwa awali na kupangapanga vitu tayari kwa usiku kuhamia makazi mapya, Magomeni. Niliwaambia wapangaji wenzangu wote, nao wakanitakia maisha mema huku wakisema tukumbukane kwani hata wao walikuwa kwenye mchakato wa kuhama kwenye nyumba ile.
***
Saa mbili usiku nilikuwa juu ya lori tukipeleka mizigo makazi mapya, lakini moyoni nilikuwa na maswali mengi ambayo mpaka leo hii siyakumbuki na yalikosa majibu. Pia, nilijikuta nakosa amani ya moyo na sikujua ni kwa nini!
Nje, nilikuta taa inawaka, ndani pia taa inawaka, lakini si sebuleni bali kwenye korido. Hii iliashiria kwamba, wale wapangaji wenzangu walisharudi kutoka kwenye biashara zao.
Nilishusha vyombo kwa kusaidiwa na wasaidizi wa dereva wa lile lori, lakini nilishangaa sana kuona kila nikiingia na mizigo, wale wapangaji wenzangu wanacheka sana chumbani kwao. Maana yangu ni kwamba, kwa kawaida walitakiwa hata watoke na kunisalimia ili tufahamiane. Tena kwa wengine, mume angetoka na kunisaidia kubeba hata stuli tu.
Ilifika mahali, wale vijana waliokuwa wakinisaidia waliniuliza:
“Hivi hao majirani zako mbona hawatoki, wanacheka tu chumbani.”
Niliwajibu mimi mwenyewe sijui, lakini sikumaindi sana. Akaja mama mmoja aliyesema anaishi nyumba ya pili, akasalimia na kuniuliza maswali.
“Hamjambo wanangu?”
Tuliitikia wote, akauliza nani anahamia pale kati ya sisi wote, tulikuwa watano mbali na dereva.
“Ni mimi.”
“Ooo, mzima baba?”
“Mimi mzima mama.”
“Unaitwa nani?”
“Humuli Samaki.”
“Unahamia peke yako au uko na mke na watoto?”
“Peke yangu mama.”
“Humuli Samaki ni mwenyeji wa wapi?” 
“Usukumani.”
“Haya, naamini uliaga wakati unaondoka nyumbani.”
“Hilo lilikuwa la kwanza mama.”
“Haya, kila la kheri.”
Tuliendelea na kazi ya kuingiza vyombo ndani hadi tukamaliza. Wale wenye gari wakaondoka, nikabaki mimi peke yangu.
Nilijiwekea malengo kwamba, nihakikishe naweka sawa kila kitu ili kesho yake nisiwe na kazi hiyo zaidi ya kwenda kazini. Niliifanya kazi kwa muda wa saa tatu, mpaka kwenye saa saba na nusu usiku nikamaliza.
Nilibadili nguo, nikavaa taulo na kwenda kuoga. Nilikuta bafu limetoka kutumika kama dakika kumi nyuma, sikushangaa kwani si kuna wapangaji wengine ambao tulitakuwa tunatumia bafu moja.
Usiku kabla ya kuzima taa, nilizima taa, nikapanda kitandani. Kabla sijapata usingizi, niliwasikia wenzangu wakicheka sana na kuongea huku wameweka muziki. Lakini ule muziki haukuwa wa kiarabu, kizungu wala kiswahili.
Hata maongezo yao, mimi nilisikia sauti tu lakini kusema walikuwa wanatumia lugha gani si rahisi. Kuna wakati kama walikuwa wakiongea kihindi, pia niliwasikia kama wanaongea kiarabu, nikajua ni watu wa namna hiyo.
Lakini sikulala mpaka nikampigia simu dalali kumuuliza kama wale wapangaji wenzangu ni weupe au waswahili kama mimi, akasema hata yeye hajui kwani hakuwahi kuwaona hata siku moja.
Basi, nililala. Asubuhi niliamka nikiwa nimechoka sana. Wakati nakwenda bafuni kuoga niligundua ni mimi peke yangu ndiye niliyekuwa nimetangulia kuamka, kwani bafuni hakukuwa na maji yaliyomwagika kwa muda huo.
Baada ya kuoga nilirudi chumbani kwangu kujiandaa kwenda kazini. Wakati najiandaa, nilisikia mlango ukifunguliwa, nikajua ni wenzangu wanakwenda kuoga au chooni kama ilivyo kawaida kwa wanadamu wakiamka asubuhi.
Niliamua kutumia nafasi hiyo kuwatambua. Nilivizia pale niliposikia mlio wa maji bafuni na mimi nikatoka kwenda kupiga mswaki kwa mara ya pili. Sehemu niliyosimama, mtu akitoka bafuni kwenda ndani ilikuwa lazima nimuone kwani ilikuwa kiasi cha kugeuka tu.
Lakini cha kushangaza, nilikuwa sisikii maji kumwagika, nikageuka na kuona mlango wa bafuni upo wazi. Mbali na mlango kuwa wazi, pia chini nikaona alama za kandambili nne zikiwa zimekanyaga, nikajua wametoka.
“Lakini wamepitaje hapa?” nilijiuliza.
Nilirudi ndani, mlangoni kwao nilikuta kandambili pea mbili zikiwa bado na majimaji kwa mbali, jambo hili lilinifanya nijiulize sana.
Nilijipa ujasiri na kuamua kuchungulia ndani ya chumba hicho kwa kutumia nafasi ya katikati ya mlango ambapo niliweza kuona hadi kitanda lakini sikumwona mtu mwingine.
Niliingia kwangu, nikaweka mswaki, nikavaa vizuri na kuondoka zangu. Nilitegemea wenzangu nimewaacha ndani, kwani nilipofika mlangoni nilikuta umefunguliwa na upo wazi. Nilirudi ndani hadi kwenye mlango wao.
“Wa ndugu,” niliita kwa sauti.
“Jamani wa ndugu.”
Ukimya ndiyo ulinifanya nibaini walishaondoka. Kwani kulikuwa kimya sana na kandambili zilikuwa pembeni ya mlango si pale pa kwanza.
Nilifunga mlango mkubwa nikaondoka, mbele nilimwona yule mama aliyekuja usiku kuniuliza maswali. Alikuwa amesimama nje ya nyumba yake, aliponiona akashutuka na kuita majina mawili ya watu. Wakatoka watoto wake wawili, ni mabinti wenye miaka kama kumi na nane na ishirini na mbili hivi.
“Hujambo kijana?” yule mama alinisalimia kwa furaha.
“Sijambo mama, shikamoo.”
“Marhaba.” Kisha akawaambia kitu wale watoto wake nao wakanikazia macho.
“Mama umewaona majirani zangu hapa?”
“Majirani zako akina nani?”
“Wapangaji wenzangu.”
“Kijana, kua uyaone ya dunia. We si umeshakua, utayaona ya dunia.”
Kauli hiyo iliniogopesha sana, nikashtuka na kumuuliza mama.
“Mama una maana gani?”
“Sisi hatutaki umbeya kijana.”
“We si umeambiwa utayaona kwa hiyo subiri tu,” alidakia binti yake mkubwa.
Miguu ilitetemeka, mwili uliisha nguvu, nikajikuta nataka kukaa, lakini sikuweza. Nilichoamua ni kuondoka huku nampigia simu yule dalali.
“Vipi hujambo bwana?”
“Mimi sijambo.”
“Za makazi mapya.”
“Si nzuri bwana.”
“Kwa nini tena?”    
“Sielewielewi.”
“Kivipi?”
“Kuna mambo kama si ya kawaida.”
“Yapi hayo?”
“Wale wapangaji wenzangu siwaelewi kabisa.”
“Kivipi?”
“Ah! Watu gani mimi mgeni nimehamia washindwe kutoka kunisalimia ili angalau tufahamiane?”
Dalali alicheka sana kisha akasema:
“Wale ndivyo walivyo bwana, si unajua tena malezi, mwingine kalelewa vile, mwingine hivi. Ila ulichokisema ni kweli, haiwezekani nyumba mnayoishi mpate mgeni halafu msitambuane, sasa mkikutana njiani je?”
“Si ndiyo hapo sasa,” nilisema nikijifanya lawama zangu ni kwa ajili ya hilo tu, lakini kumbe nilikuwa na zaidi ya hapo.
Kazini siku hiyo nilishinda sina amani, sina raha, mwili ulikuwa kama umetoka kufanya kazi nzito ambayo sijawahi kuifanya kwa siku nyingi, wenyeji wa Pwani wanaita mavune.
Kwa upande mwingine nilitamani sana jioni ifike ili nikaone siku hiyo kitatokea kitu gani kipya kwenye nyumba ile. Jioni ilifika, nikaondoka kazini, sikutaka kupitia popote, dukuduku langu lilikuwa kwenda nyumbani tu.
Nilichukua kama saa moja kutoka kazini hadi kufika nyumbani. Nje nilikuta mfuko wa rambo  mweusi, ndani yake ulionekana kuwa na kitu kwani ulikuwa umetuna sana. Niliinama kuipekenyua ili nijue ndani kulikuwa na nini, nilishangaa kuona ni vipande vya nyama za kuchoma tena vilikuwa vya moto.
“Kha! Atakuwa nani ameweka?” nilijiuliza mwenyewe, nikauacha palepale, mimi nikapanda ngazi za kuingia ndani. Mlango ulikuwa wazi hali iliyoashiria kwamba, wenzangu walisharudi. Nilisukuma mlango, nikaingia. Nilikutana na harufu ya pafyumu, nikahisi walikuwa wakijiandaa kutoka.
“Jamani za leo?” nilisalimia kwa sauti ya juu licha ya kwamba, mlango wao ulikuwa umefungwa, hakuna aliyeniitikia, hilo sikulijali sana kwani niliamini kwa kuwa walikuwa ndani, isingekuwa rahisi wasikie salamu yangu.
Niliingia sebuleni kwangu, kisha nikaenda chumbani, kuna kitu kilinishangaza, nikasimama kwa mshtuko. Nilikuta sehemu nilipoweka kiberiti asubuhi siyo, nilikiacha juu ya meza, nikakikuta juu ya kitanda. Niliacha kioo na kitana juu ya kitanda, lakini nikavikuta kwenye stuli, niliguna!
Nilikishika kioo na kukiangalia kwa umakini kama kina mabadiliko yoyote, lakini sikuona, nikashika kitana. Nilipokigaua sana pia sikuona kitu cha tofauti, nikaamua kuchania, nikahisi kuguswa na kitu kama nywele ndefu kama za mtu aliyefuga. Nilikiweka kitana juu usawa wa dirishani, nikaona nywelenywele nene, nyeusi, mwili wote ukasisimka.
Ninavyojua mimi, mwanamke mwenye nywele nyingi akichania kitana, ndiyo huacha nywele, sasa mimi nilikuwa na nywele fupi sana zisingeweza kuacha nywele ndefu kwenye kitana.
“Mh! Hapa kuna kinachoendelea,” nilisema moyoni huku nikikaa. Nilishtuka zaidi kuona soksi zikiwa kwenye msumari nyuma ya mlango wakati niliacha chini.
“Huyu ni nani?” niliuliza kwa sauti ya ukali.
Ghafla nikasikia kicheko kutoka chumbani kwa wale wenzangu.
Nilikaa kwenye kochi, nikaanza kuangalia sehemu mbalimbali za mle ndani ambazo niliamini naweza kuona mabadiliko mengine mbali na yale ambayo nilishayaona, lakini sikubahatika.
Nilitoka, nikaenda sebuleni ambako nako nilianza kuangalia kila kona ya sebule. Nilishangaa kuona glasi ya maji ya kunywa ambayo niliitumia asubuhi kisha nikaacha maji yamejaa, ikiwa haina hata tone la maji mbaya zaidi, iliwekwa juu ya kabati ambapo mimi niliiweka kwenye meza ya katikati ya sebule.
“Mh! Hii kali sasa,” nilijikuta nikisema kwa sauti, mara nikasikia kicheko tena kutokea upande wa pili kule kwa wenzangu. Sasa nikaanza kama kuhisi kitu kuhusu watu hao. Ni kwa nini kila nilipoongea kwa sauti ndipo na wao waliangua kicheko?
Niliamua kujaribu tena, nikasema kwa sauti:
“Nitakuja kuua mtu, kweli tena.” Nikasikia kicheko tena, safari hii kilidumu kwa muda.
Moyoni nikasema naanza kufanyia kazi uhusiano wa maneno yangu na vicheko vya wale majirani. Nilitoka kurudi chumbani, wakati napita kwenye korido, nilisimama jirani na mlango wao. Walikuwa wakiongea, lakini niliposimama mimi, kukawa kimya ghafla kama hakuna watu.
Nilipozama chumbani, nyuma wakaanza kuongea tena. Sikufunga mlango ili niweze kusikia wanachokiongea, lakini jamani kwa kusema ule ukweli wa Mungu, sikujua walikuwa wakitumia lugha gani katika kuwasiliana hata pale nilipojitahidi kutega masikio kwa umakini wa hali ya juu sana.
Kuna wakati utadhani wanatumia sana neno dotikom, lakini ukisema usikilize zaidi unasikia wakisema sana kotoko au kiburate, wakati mwingine sauti ya kike ilisema kaunto, ya kiume ikarudia hivyohivyo, kaunto.
Nia yangu kubwa ilikuwa kuwaona kwa sura na kufahamu kama ni ngozi nyeusi au nyeupe. Hilo peke yake lingenipa mwanga ni watu wa aina gani naishi nao pale ndani ya nyumba.
Nilisikia mlango wa chumbani kwao ukifunguliwa na mimi nikatoka haraka sana, cha ajabu sikuona mtu akitoka lakini mlangoni kulikuwa na kandambili pea moja tu wakati zilikuwa pea mbili.
Hilo lilimaanisha kwamba, mmoja wao alitoka kwenda chooni, nilichofanya ni kuamua kusimama katikati ya mlango wangu ili huyo aliyekwenda chooni akirudi nimuone. Ni kweli mmoja wao alikwenda chooni kwani nilisikia mlio wa maji.!!
NilijiTahidi kusimama mlangoni kwangu kumsubiria. Kwa ramani ya nyumba ile ilivyo, asingeweza kutoka chooni bila mimi kumwona hata kama angekuwa anataka kutoka kwenda nje au uani.
Mlio wa maji ulikosa kusikika, nikawa natumbulia macho kule huku moyoni nikisema:
“Leo ndiyo leo, asemaye kesho mwongo, hata afanyaje, hawezi kunichenga hapa hata kidogo,” nilisema moyoni, ingawa wakati huo mapigo ya moyo yalikuwa yakinienda kwa kasi.
Nilipoanza kuhisi muda unakwenda na hakuna mtu aliyetoka, nikampa dakika tatu kwamba lazima atakuwa anavaa ndiyo maana anachelewa:
“Labda alikuwa anajisaidia haja kubwa, maana wengine huwa wanavua nguo zote, lakini mimi nipo, siendi kokote,” nilisema moyoni nikiwa bado nimesimama mlangoni kwangu.
Baada ya muda, nikasikia watu wakiongea chumbani kwao, nikashtuka, nilijikuta nikisema:
“Haa!”
Haraka sana nilitupa macho mlangoni kuangalia kandambili, nikazikuta pea mbili, nikashangaa:
“Ina maana amenipita hapahapa au? Haiwezekani, asingeweza kunipita hata kama ingekuwaje?” niliwaza. Nilitoka kuelekea chooni, nikakuta mlango uko wazi, nikachungulia ndani, hakukuwa na mtu, nikanyoosha mikoni, nikarudi ndani.
Nilifikia kwenye kochi sebuleni, nikahema kwa nguvu kwani niliamini nimo ndani ya miujiza mikubwa ya ndani ya nyumba ile.
“Hivi ni kwa nini dalali alinidanganya hivi?” nilijiuliza mwenyewe nikiamini kwamba, dalali aliyenipangisha nyumba ile alijua mchezo mzima ila alitaka kupata fedha tu ndiyo maana alinipangisha bila kunipa tahadhari.
Nilitoka sebuleni, nikaenda chumbani, kitandani nikakuta ‘toilet paper’ ikiwa imekatwa sehemu. Mimi niliicha pembeni ya dirisha, lakini ikaonesha kuna mtu aliichukua na kunyofoa kidogo kisha badala ya kuirudishia palepale, yeye aliiacha kitandani.
Mbali na ‘toilet paper’ pia kuna kikopo chenye vijiti vyenye pamba za masikio kilikuwa kwenye stuli jirani na kitanda, lakini kwa muda huo kilikuwa kimeanguka chini halafu vijiti vimebaki kama vitatu tu kwa maana kwamba, aliyeingia kuchukua ‘toilet paper’ ndiye huyohuyo aliyechota vijiti vya pamba.
Nilianza kuhisi kuwa sikuwa kwenye nyumba salama, lakini kwa uthibitisho upi? Moyoni nikasema nitajua tu, mimi ndiyo mimi.
***
Nilikaa ndani kwangu hadi usiku ulipoingia, nikasema nibadili nguo kwa kuvaa bukta na singilendi halafu nitoke kwenda kula gengeni kwani siku hiyo sikuwa najisikia kupika chochote. Ni mara nyingi nilipenda kula gengeni.
Nilitoka, nikasimama mlangoni ili nifunge mlango wa chumbani, nilipoangalia chini, upande wa wenzangu nilikuta nje ya mlango wao pana vijiti vya pamba za masikioni vikiwa vimetumika, nikiwa katika mshango, mbele nikaona tishu ikiwa imefutiwa majimaji yenye rangi nyekundu kama damu.
Nilitembea kwa wasiwasi, nikatoka nje, sikufunga mlango kwa funguo, lakini niliubamiza tu, funguo nilikuwa nazo, nikaenda gengeni kula. 
Pale kwenye genge ambapo si mbali sana na nyumbani, alikuja yule mama aliyeniuliza mimi ni mtu wa wapi, nilimsalimia, lakini kabla hajaitikia alishtuka kuniona.
“Upo kijana wangu?”
“Nipo mama, nimetoka kazini nimekuja kupata kidogo.”
“Pole sana, uoe sasa.”
“Huo ndiyo mpango wangu mama.”
“Ee, uoe halafu mimi nitakupa vyumba viwili pale kwangu, nakuahidi.”
“Nashukuru sana mama. Naanza kujipanga.”
“Sawa, vipi wenzako lakini?”
Nilisita kumjibu, nikabaki namwangalia tu, naye alibaini kwamba nimepata mshtuko na swali lake.
“Vipi wapangaji wenzako, naamini utakuwa hujaonana nao?”
“Ni kweli mama, tena hebu nakuomba kidogo,” nilisema nikienda pembeni kidogo ili na yeye anifuate tukaongee.
“Niambie,” alianza kusema.
Nilimuuliza kama kuna anachokijua chochote kile kuhusu wale wapangaji wenzangu. Alianza kwa kusema:
“Kusema ule ukweli sina kwa undani, ila napenda kukwambia kwamba, unaishi na watu ambao unahitajika moyo wa ziada ili uweze kuendelea kuishi nao.
“Pale mbali na wewe, pameshakaa wapangaji wengine saba, tena wote kama wewe, hawajaoa. Lakini kinachoshangaza ni kwamba, wanaondoka baada ya wiki mbili, mmoja aliondoka baada ya siku tatu tu.”
“Kwa hiyo hakuna hata mmoja aliyewahi kukwambia ameona nini kule ndani?”
“Hakuna.”
“Lo! Mimi mama mambo ninayoyaona yanatisha.”
“Kama mambo yapi, nisimulie kidogo.”
Nilipotaka kuanza kumsimulia huyu mwanamke, ghafla alitokea msichana mmoja, mweupe, mrefu kiasi, amejazia sehemu mbalimbali za mwili, akaguna na kusema:
“Kaka Humuli mambo vipi, za siku?”
Nilipata kigugumizi kikubwa kumjibu mambo poa kwani sikumjua na sikuwa nakumbuka chochote kuhusu yeye, sura yake ilikataa kichwani mwangu.
“Wewe ni nani kwani?” nilimuuliza.
Akaachia tabasamu kwa mbali, uzuri wake ukaongezeka.
“Ha! Humuli, hunikumbuki mimi, kweli?”
“Sikukumbuki hata kidogo.”
“Sasa we binti, kama wewe ndiyo unamkumbuka si umkumbushe mlionana wapi?” yule mwanamke alisema kwa sauti ya mshangao.
Lakini yule msichana mrembo alimwangalia yule mwanamke kwa macho yaliyojaa hasira…
“Mama uhusiki.”
“Najua, lakini unapoteza muda kwa kuzungushazungusha wakati kumbe wewe unamkumbuka, yeye umeshajua hakukumbuki na amekwambia tayari.”
Nilishangaa kumwona yule msichana akibetua kichwa kama aliyekuwa akiweka vizuri nywele zake, ghafla yule mwanamke niliyekuwa naye akajishika kichwa na kulalamika kinamuuma sana.
“Jamani kichwa! Kichwa jamani, daa!”
“Vipi mama, imekuwaje kwani?” nilimuuliza.
“Kichwa Humuli, kinavuta ghafla! Uwiii.”
Nilianza kuogopa, nilihisi naangukiwa na msala maana akifa pale na watu waliona nikienda naye pembeni si nitahojiwa mimi?
“Kwani mama una kawaida ya kuumwa kichwa?” nilimuuliza nikimsogelea ambapo yeye sasa alikuwa ameinama.
“Sina, ndiyo nashangaa hapa.”
Niliona hakuna dawa nyingine zaidi ya kumpeleka kwake ili nikaungane na familia yake kumpeleka hospitali. Lakini kabla ya kufanya hivyo niliinua macho ili nimwambie yule dada anisaidie na kama anataka kunikumbusha, hayo yangefanyika baadaye.
Ile naanaza kusema anti huku nikiwa nimeinua macho, nilishangaa kutomwona yule msichana pale.
“Khaa!” nilijikuta nikisema hivyo.
“Mama twende nyumbani ili tukupeleke hospitali na watoto wako.”
“Ha! Mbona kimeachia,” alisema akionekana kushangaa na kuniangalia, alikuwa amepanua kinywa. 
“Kweli?”
“Eee, niko mzima kabisa.”
“Au?” nilitaka kusema neno lakini zikulimaliza, nikahisi ulimi unakuwa mzito si kwa kushikwa bali kwa matakwa yangu.
“Humuli.”
“Naam.”
“Ni kweli yule binti humjui?”
“Simjui mama.”
“Kuna mawili hapo, humjui au humkumbuki.”
“Vyote mama, simkumbuki na pia simjui.”
“Lakini wewe si alikutaja kwa jina?”
“Mwenyewe nilishangaa sana.”
“Basi Humuli nimeshaelewa, kwaheri, nimeelawa ni kwa nini nimeugua kichwa na yule ni nani, pole sana wewe kijana,” alisema yule mwanamke huku akiondoka zake kuelekea kwake.
Nilimtazama, lakini baadaye nilirudi kwenye kibanda cha chipsi.
“Mzee nakuona na miss jini,” muuza chipsi mmoja alisema.
“Yupi, yule mwanamke?”
“Hapana, yule msichana.”
“Mi simjui, kwani anaishi wapi? Maana kasema ananijua, ameniita na jina.”
 “Khaa! Kumbe wewe kama sisi. Huyu dada anaishi mitaa hiihii, lakini hakuna hata mmoja anayejua nyumba anayoishi! 
“Kuna jamaa mmoja anaitwa Maleke, Maleke aliwahi kumfuatilia kwa nyuma lakini alishindwa kujua aliingia nyumba gani!” 
“Mh! Au jini?” niliuliza kwa mshtuko mkubwa.
“Ndivyo watu wanavyosema, sasa alipokuja kusimama na wewe, tukawa tunabishana, wengine wanasema ni miss jini, wengine siye, lakini alipokuwa anaondoka tukagundua ni miss jini.”
Basi, tuliishia hapo, nikachukua chipsi zangu na kwenda nazo nyumbani, niliamua kwenda kulia kule.
Nilifika, nikasukuma mlango mkubwa nikazama ndani kwangu. Lakini wakati napita kwenye usawa wa chumba cha wale wenzangu nikasikia vicheko, tena vicheko kwelikweli.
Sikuwajali, nikaingia sebuleni kwangu, nikafunga mlango kwa ndani, nikaweka chipsi juu ya meza, nikaenda pembeni ya chumba ambako kuna ndoo ya maji ili nichote ya kunawa.
Wakati naanza kula nilihisi na kugundua kitu. Niligundua mabakimabaki ya chipsi na kuku juu ya meza yangu wakati ukweli ni kwamba, tangu nimehamia pale sikuwahi kula chipsi wala kuku.
“Humu ndani kuna mtu anaingia kufanya mambo yake, lini mimi nimekula chipsi na kuku humu ndani?” nilijiuliza, nikasikia kicheko kutoka kwa wenzangu.
“Haa! Haaa! Ha! Haaaa…aaaa.”
Niliinua macho kuangalia juu kwenye ‘silingbodi’ kama vile niliyekuwa nimeona kitu, akili yangu ikawaza kitu cha dakika chache nyuma, nacho ni hiki:
“Humuli.”
“Naam.”
“Ni kweli yule binti humjui?”
“Simjui mama.”
“Kuna mawili hapo, humjui au humkumbuki.”
“Vyote mama, simkumbuki na pia simjui.”
“Lakini wewe si alikutaja kwa jina?”
“Mwenyewe nilishangaa sana.”
“Basi Humuli nimeshaelewa, kwaheri, nimeelawa ni kwa nini nimeugua kichwa na yule ni nani, pole sana wewe kijana.”
Nilianza kuamini kwamba, kuna uhusiano mkubwa kati ya yule msichana na wale wapangaji wa pale ndani nilipo, inawezekana alinijua jina kwa sababu naishi nao na wana uwezo wa kujua jina la mtu kulingana na mazingira yao.
Pia niliwaza kwamba, kuna uwezekano mkubwa yule msichana alitokea baada ya maono yao kuniona mimi na yule mama wa jirani tukitaka kuwazungumzia wao kama wapangaji wenye maajabu hivyo hawakupenda iwe hivyo ndiyo maana msichana akaibuka na kusababisha mvurugano.
“Itakuwa kweli, ndiyo maana yule mama naye alisema ameshajua ni kwa nini aliugua kichwa ghafla, alijua yule msichana ni nani na kwa nini yeye kasikia maumivu ya ghafla vile.”
“Lakini pia kuna wale wauza chipsi, nao niliwakumbuka hasa yule mmoja aliyesema yule msichana wanamjua, anaishi mtaani, lakini hawajawahi kubaini anaishi nyumba gani na kwa mzee nani wala anajishughulisha na nini,” hayo yote niliyawaza mimi.
Nilisimama, nikachukua sabuni ya kuogea ambayo haijafunguliwa, nikaipiga chini kwenye kapeti  kwa hasira huku nikisonya, nikasema kwa sauti ya chini:
“Humu ndani naishi na majini.”
Kule chumbani nikasikia wakicheka.
“Si unaona, nimesema mimi, lazima naishi nao humu ndani, da! Najuta sana,” nilisema. Kicheko kikasikika tena, safari hii kilikuwa cha juu zaidi kuliko kile cha awali.
Moyo ulijaa mawazo, akili ilihisi uchungu wa maisha, niliwaza fedha nilizozilipa kwa ajili ya kupanga mle ndani, nikamkumbuka dalili, niligundua alichofanya ni kunitapeli na hakuna lingine wala hakuwa msaada kwangu.
“Mimi ni mwanaume, kama niliweza kupata fedha za kupanga hapa, sishindwi kupata nyingine za kupanga sehemu nyingine tena mbali na hapa,” nilisema kwa moyoni.
***
Usiku nikiwa nimelala, nilichelewa sana kupata usingizi, ghafla nikaona taswira za watu ukutani, wawili tena wakiwa wamesimama, ni mwanamke na mwanaume. Niliogopa sana, nikainua kichwa polepole kuwaangalia kwa umakini, japo kulikuwa na giza, lakini niliweza kuona vizuri lakini si kwa uwazi mkubwa kama ambavyo taa ingekuwa inawaka. 
Ni kweli walikuwa watu wawili kama nilivyoona, tena weupe nikimaanisha si watu weusi. Walikuwa wakionesha vitendo vya kucheka huku wakijinyonganyonga.
Kuna wakati walitembea mpaka jirani na kitanda changu kisha wakageuza na kurudi pale ukutani. Nilipeleka mkono hadi kwenye swichi ya kitanda (bed switch), nikawasha, cha ajabu sikumwona mtu wala dalili pale ukutani. 
Niliamka nikiwa nahema kwa kasi mpaka nikajishika kifuani, nikafungua mlango na kutoka nje ili nijifanye nakwenda chooni lengo langu lilikuwa kupata picha kwa wenzangu kukoje maana niliwashuku wao na wale walioonekana chumbani kwangu.
Kwa wenzangu niliwasikia wakikoroma kwa zamu. Nikajiuliza ina maana si wao waliokuja chumbani kwangu? Niliona ni utani wa hali ya juu.
Niliamua kurudi chumbani na kukatisha safari ya kwenda chooni, nikafunga mlango wangu kwa funguo na kupanda kitandani, nilizima taa ili nione kama yale mauzauza yatatokea tena.
Ukimya ulitawala kwa muda bila kujitokeza chochote, nikaanza kupitiwa na usingizi kwa kusinziasinzia, ghafla ukutani nikawaona tena wale watu wawili. 
Safari hii walikuja hadi kitandani, wakakaa, wakasimama, wakaenda kwenye kabati, wakafungua, wakatoa mashuka na kujifunika, wakayarudisha, wakaenda nyuma ya mlango, wakatungua mashati yangu mawili, wakagawana na kuyavaa kisha wakayavua, mmoja mwanaume akaenda sehemu yenye redio, akapeleka mkono, nikajua anataka kuiwasha, lakini hakufanya hivyo.
Nilichoamua kukifanya akilini ni kuwasha taa kwa ghafla na kuwavamia na nilipanga kumvamia mwanamke nikiamini ndiye aliyekuja kule kwenye chipsi. Polepole nilipeleka mkono hadi kwenye swichi, nikawasha taa kwa ghafla huku macho yangu yakiwa kwao, lakini sikumwona hata mmoja! Kwangu haikuwa mapambano bali nilichukulia kama changamoto za maisha.
***
Asubuhi, niliamka nikiwa nimechoka sana, lakini kabla sijatoka kitandani nilisikia nje ya mlango kukiwa na hali ya watu kutembeatembea tena kwa kasi, niliinua shingo ili nione kama nitasikia zaidi, lakini kukawa kimya.
Niliamka, nikatoka, nilikwenda sebuleni kwanza kuangalia kama kuko salama. 
Nilishangaa kukuta mezani kuna mfuko wa rambo uliojaa chipsi kuku kama nilivyonunua mimi, lakini zangu nilikula, sasa zile sikujua zilitoka wapi. 
Niliubeba ule mfuko nikatoka nao, nilifungua mlango mkubwa wa nje nikautupia pembeni kidogo, niliporudi, nikaenda chooni, mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani kwani hata niliposhika kitasa na kukivuta kilikuwa kigumu.
 Hii iliashiria kwamba kuna mtu, kwa hiyo moyoni nilisema nisimame palepale nje ya mlango hadi atoke. Nilisimama eneo ambalo akitoka tu, uso kwa uso na mimi.
“Tuone leo, wao si wajanja, leo nimemnasa mmoja wao,” nilisema moyoni.
Dalili zote zilionesha kwamba mle chooni mlikuwa na mtu kwani niliweza kusikia hata kuhema kwake, mara mlio wa maji, mara alikohoa, tena kwenye kukohoa nikabaini mtu mwenyewe alikuwa ni mwanamke ndiye aliyekuwa mle.
“We kohoa mpaka utapike, lakini mimi nipo hapa mpaka utoke,” nilisema moyoni.
Nilikaa sana, ikafika mahali nikachoka, lakini moyoni nikasema siondoki hata iweje, lakini nilishtuka kitu, niligundua muda mrefu sijazisikia zile dalili kama maji au kuhema, nikafunguka akili.
“Mh! Siyo kwamba ametoka?”
Ile namalizia kusema ‘ametoka?’ nikasikia kicheko kutoka kwenye chumba chao. Vicheko vikubwa sana cha kike na kiume.
Nilirudi chumbani mwili ukinisisimka, hapo ndipo niliamini mia kwa mia kwamba, nilikuwa nadili na watu wasiokuwa wa kawaida.
Niliingia chumbani, nikampigia simu dalali.
“Haloo,” niliita.
“Haloo. Halooo,” nilirudia lakini sikupokelewa.
Nikiwa nimeachana na simu, mara iliita yenyewe, alikuwa ni dalali nikapokea.
“Haloo,” niliita.
“Haloo,” niliitikiwa lakini sauti haikuwa ya dalali.
“Mzima bwana?” nilisalimia.
“Tuone leo, wao si wajanja, leo nimemnasa mmoja wao.”
Ha! Nilishtuka sana, nilisikia sauti yangu mwenyewe ikisema hivyo. Ikaendelea.
“We kohoa mpaka utapike, lakini mimi nipo hapa mpaka utoke.”
Nilikata simu, nilikuwa nahema sana, mapigo ya moyo yalikuwa yakienda kwa kasi ya ajabu huku nikishindwa kuona sawasawa.
“Hii ni hatari sasa,” nilisema.
***
Usiku wa siku hiyo sikulala kusema kweli kwani kila nilipofikiria maisha yale sikuona sababu ya kuendelea kuishi pale. Moyoni nilisema kwamba, ni afadhali ningeishi na watu ambao ni majambazi kuliko hawa, nafuu ningepanga nyumba moja na makahaba kuliko kupanga nyumba moja na majini.
Nilichoamua, asubuhi nikifika kibaruani tu niombe ruksa kisha nianze kumsaka yule dalali na pia nitafute dalali mwingine ambaye atanitafutia vyumba kwingine na si maeneo yale tena kwani niliyaona yana nuksi.
***
Asubuhi kulikucha salama kabisa, tena usiku wa siku hiyo sikuona mauzauza wala dalili zake. Nilikwenda kuoga bila kukagua mazingira, moyoni nilisema liwalo na liwe kwa maana kwamba, wawepo wasiwepo sawa tu.
Bafuni niligundua wameshaoga kwani kulikuwa na majimaji ya muda mfupi uliopita. Nilipomaliza kuoga, nilijiandaa na kutoka. Nje nilikutana na mtu ana mkokoteni, akanisalimia.
“Za asubuhi bwana mkubwa?”
“Salama, karibu sana.”
“Asante, kuna watu fulani wanaishi humu nina shida nao.”
Aliposema hivyo nilishtuka sana, niliamini yeye ni mmoja wa wale ila amejigeuza kwa kujifanya ana shughuli za mkokoteni.
“Unawajua kwa sura?” nilimuuliza huku nikiwa na wasiwasi maana alinikazia macho.
“Siwajui.”
“Sasa una shida nao kivipi watu usiowajua kwa sura?”
Ni kwamba, kuna binti mmoja huwa wanamtuma niwaletee maji, nikifika hapa huyo binti anabeba madumu kupeleka ndani, sasa jana nilikutana na huyo binti nikamuuliza kuhusu malipo yangu ya mwezi sasa, akasema nije nifuatilie mwenyewe.”
Nilishangaa sana kusikia hivyo. Nijuavyo mimi mle ndani mna watu wawili, mwanamke na mwanaume, sasa kama kuna binti hilo lilikuwa jipya kwangu, labda lakini.
“Huyo binti naye anaishi humu au?” nilimuuliza.
“Sidhani, inaonekana kama huwa wanamtuma tu.”
“Kwa nini huamini kama anaishi humuhumu ndani? Hafanani na wao wenyewe?” hili swali niliuliza likiwa na mtego mkubwa sana, nilitaka nijue uhalisia wake.
“Siwezi kusema hafanani wakati wao siwajui kwa sura.”
Hapo ndipo nilipopataka, nilidhani atasema hafanani nao, ningejua ni walewale.
“Oke, nadhani wameondoka kwenda kazini.”
“Ah! Sasa mimi fedha zangu nitazipataje jamani?”
“Subiri wakirudi jioni.”
“Wewe utakuwepo?”
Nililishangaa swali hilo, hakuwa akinidai mimi lakini anataka niwepo?
“Unataka niwepo?”
“Ee.”
“Kwa nini?”
“Naamini utanisaidia kuzipata fedha zangu.”
“Uliwahi kuja wakagoma kukupa?”
“Siyo hivyo, ila kila nikija, nikigonga mlango huwa hawafungui.”
“Basi nitakuwepo.”
“Asante kaka. Nije saa ngapi?”
“Saa moja nitakuwa nimerudi.”
Aligeuza mkokoteni na kuondoka zake huku akisema:
“Muda huo nitakuwa nimefika kaka.”
Niliondoka kwenda kazini kuomba ruksa. Lakini wakati naondoka, mfanyakazi mwenzangu mmoja aliniuliza nakwenda wapi, nikaamua kumsimulia kwa ufupi kisa changu.
“Kha! Sasa hapo tatizo liko wapi, mbona dawa ipo rahisi sana.”
“Rahisi! Ni ipi hiyo?”
“Sikia, twende pembeni nikakusimulie,” aliniambia yule mfanyakazi mwenzangu huku akiangalia kulia na kushoto kama mabosi watatokea.
Tulikwenda kusimama pembeni, akaanza kuniambia:
“Sikiliza, kama unaishi nyumba ya namna hiyo, unachotakiwa kufanya, kila siku asubuhi na jioni au usiku unapuliza bangi ndani ya nyumba, kama ni majini, mapepo sijui nini, utaona mambo poa kabisa.”
Sikuamini maneno hayo, nikamuuliza mara mbilimbili kama ni kweli.
“Khaa! Nina mjomba’ngu aliwahi kuishi kwenye nyumba ya hivyo, akaenda sehemu akaelekezwa dawa ni hiyo, akaitumia, mpaka sasa anaishi kwa raha hakuna cha majini wala mapepo,” alisema.
Nilimsikiliza nikianza kuamini kwa mbali, lakini nilifika mahali nikamuuliza hiyo bangi mimi nitavuta au nitaiwasha ili itoe moshi yenyewe?
“Ukishaiwasha, utaiweka mezani au popote ndani kwako, lakini angalia isizimike ili moshi wake usambae chumba kizima au sebule nzima.”
“Hilo linawezekana,” nilimwambia nikimtumbulia macho.
Kwa sababu nilikuwa nimeshaaga, ilibidi niondoke tu na kurudi baadaye. Nilikwenda mtaani, nilitafuta bangi nikapata maeneo ya Kariakoo, nikaitia mfukoni.
Nilizurura sana siku hiyo, saa tisa kamili nilikuwa njiani narudi kazini. Nilipiga hesabu za kufika kazini na kuondoka, maana muda wa kazi ni saa tisa na nusu.
Wakati napita pale Kituo cha Polisi Msimbazi, fujo zikazuka, kuna machinga wawili walikuwa wanapigana kwa sababu ya kugombea sehemu ya kufanyia biashara, katika ugomvi huo mimi nilibaini mmoja wao ndiyo mwenye kosa. 
Nikampa laivu kuwa yeye ndiye mwenye tatizo, alikuja juu, akachukua boksi lenye viatu na kunirushia, likanipata kwenye bega la kulia, sikukubali, nikaokota jiwe na kumrushia, likampata mkononi.
Polisi walifika haraka sana, wakanikamata mimi, yeye na yule machinga niliyeona anaonewa, tukapelekwa Msimbazi polisi.
Tulipofika pale, afande aliyetukamata alituamuru kuvua viatu, mikanda, simu kuweka pembeni. Halafu mmoja alianza kutusachi mifukoni. Wakati tendo hilo linaanza kwa wenzangu, ndipo nikakumbuka mimi mfukoni nina vipisi viwili vya bangi.
Nilitaka kutoka mbio kituoni hapo, lakini sehemu tuliyokaa, ningesema nitoke, nisingefika nje au hata kama ningefika ningekamatwa au kupigwa risasi kama mhalifu, nilitetemeka, mwili uliisha nguvu.
Ilipofika zamu yangu kusachiwa, askari mwenyewe alishangaa kuniona nachezesha miguu kama niliyebanwa na haja ndogo, akaniuliza:
“We vipi, unaumwa?”
Nikamjibu naumwa afande.
“Unaumwa nini?”
“Sijui, nadhani homa.”
Hakunijibu, alianza kwa kutumbukiza mkono kwenye mfuko usiokuwa na kitu, akahamia wa nyuma ambao una waleti, akapeleka wa kulia kwangu ambao ndiyo wenye bangi, aliposhika, akakunja sura, alipotoa akashtuka sana na kusema:
“Haa! Hii bangi siyo?”
Sikumjibu kwani niliamini ameshaijua, wenzake waliokuwa kaunta wakaacha mambo yao na kunigeukia mimi, nao wakashangaa sana. Mmoja alikuwa amekaa juu ya stuli, akashuka huku akiniangalia kwa kunikazia macho.
“Unakuja kituo cha polisi na bangi, wewe unatutafuta nini sisi?” aliuliza yule aliyeshuka kwenye stuli.
Niliambiwa nafunguliwa kesi ya pili, ya kwanza kupigana na kujeruhi ya pili kukutwa na bangi!
Nilijitetea nikisema bangi ile si kwa ajili ya kuvuta bali nilikuwa nina shida nayo.
“Wewe usitufanye sisi watoto wadogo, tunawajua ninyi raia,” alisema yule afande aliyenisachi.
Lakini afande mmoja wa kike ambaye muda wote alikuwa akiangalia tu, akawaambia wenzake:
“Lakini huyu kaka mbona hafanani na kuvuta bangi, muulizeni ana shida nayo gani?”
Wale wenzake wakanigeukia na kuniuliza:
“Haya, wewe mwananchi, raia kabisa, unaweza kuwa na shida gani na bangi mbali na kuvuta?”
Niliwasimulia kila kitu, tena nilifika mahali nikawaambia kama kuna asiyeamini, tuongozane hadi nyumbani, Magomeni akaone maajabu ambayo hayahitaji kuelekezwa sana ili kuamini kama yapo au la!
Palipita ukimya wa sekunde kadhaa, mmoja wao akaniuliza:
“Kama ni kweli au tufanye ni kweli, ni kwa nini umemuumiza huyu?”
Nilisema kilichotokea, yule chinga niliyemsaidia naye akanitetea kwa kusema hivyohivyo, lakini afande mmoja akasema nilijichukulia sheria mkononi ambapo ni kosa kisheria.
Niliomba sana wanisamehe kwa yote, nikasingizia kwamba ni kwa sababu kichwa changu hakipo sawa kwa kuishi nyumba moja na majini.
Namshukuru mmoja wao aliniambia niondoke lakini nihakikishe situmii bangi katika kujitibu kwani serikali haiamini kama bangi ni dawa.
Nilipotoka, nilikwenda kununua nyingine, lakini akili iliingia hisia kwamba, huenda yule dada wa ajabu mle ndani ndiye anayecheza michezo ili kunikwamisha kwenda na bangi ndani ya nyumba, nikasema moyoni ngoja ninunue hii nione kitakachotokea, nikanunua tena misokoto miwili.
Nilitembea kuelekea kituo cha daladala. Njiani nilimpigia simu yule mfanyakazi mwenzangu aliyenijulisha kuhusu dawa ya kutibu nyumba yenye majini, nikamwambia sitaweza kurudi kwani nilipata wakati mgumu kidogo njiani.
Alinielewa, akaniuliza kama nimepata, nikamjibu kila kitu kimekwenda sawa, lakini sikumwambia kuhusu timbwili lililojitokeza.
Nilipanda daladala nikashuka Magomeni, niliingia ATM kutoa fedha kidogo, kisha nikatoka. Wakati natafuta mwelekeo wa kwenda nyumbani, nilimkumbuka dalali, nikampigia simu.
“Halo.”
“Halo habari za kazi bwana?”
“Nzuri, pole na kazi na wewe mwenzangu?”
“Nimepoa. Bwana vipi kuhusu nyumba?” nilimuuliza.
“Nyumba imefanyaje?”
“Si nilikusimulia matatizo yake, umesahau?”
“Kwani ulisema matatizo yake yakoje vile?”
Nilimwelezea kwa kirefu, nikafika mahali nikamwambia hadi nilivyompigia simu halafu ikapokelewa na sauti ya ajabuajabu, alicheka sana.
“Wewe bwana acha kunichekesha.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Yaani simu yangu mimi halafu apokee mtu mwenye sauti ya ajabuajabu, kwa nini sasa?”
“Mimi pia sijui.”
“We ulikosea namba.”
“Labda bwana mi siwezi kukazania sana,” nilimjibu kwa kinyongo kwani namba yake niliisevu na ninapompigia huwa nasachi jina tu, sasa nilikosea kivipi?
“Enhe, unasemaje bwana?” aliniuliza.
“Nimeshakwambia bwana.”
“Kwa hiyo unashauri nini?”
“Nataka pesa zangu nikapange kwingine.”
“Da! Hilo halitawezekana kirahisi bwana, maana mpaka nimpate mpangaji mwingine atoe fedha ndipo nikulipe wewe na mpangaji atakayekuwa tayari kutoa fedha lazima akute nyumba tupu, sasa wewe utalikubali hilo?”
“Naweza kulikubali, ila tuandikishiane.”
“Kwamba?”
“Kwamba unajikomiti nikiondoka, akiingia mpangaji mwingine tu unanilipa pesa zangu.”
“Ngoja nitakupigia,” alisema dalali na kukata simu.
Nilipokuwa nakaribia nyumbani, nikakutana na yule msukuma mkokoteni wa maji.
“Kaka za kazi?”
“Nzuri, vipi wewe?”
“Niko sawa, ndiyo unarudi?”
“Ndiyo.”
“Najua jamaa hawajarudi, nitakuja muda uleule tuliopanga.”
“Sawa, karibu sana.”
“Asante sana.”
Niliingiza funguo ili kufungua mlango, lakini nikagundua kwa ndani kulikuwa na funguo nyingine maana nilichungulia.
Nilipousukuma, ulifunguka. Hii ina maana wale watu wa ajabu walikuwa wamesharudi, wako ndani. Niliingia ndani, nikafungua mlango wa sebuleni, nikaingia humo.
Nilifikia kwenye kochi kubwa, nikajilaza. Sikuangalia kama kweli wenzangu walikuwa wamesharudi, ila nilisikia sauti ya muziki wa redio, nikajua wapo.
Mara nikasikia mlango wao mmoja ukifunguliwa, nikasikia mtu akitoka. Kwa mara ya kwanza nilisikia akisema:
“Kama utamkamata anavuta bangi apelekwe polisi, ndiyo dawa yao watu wa aina hii.”
Nilishtuka, nikakaa. Nikawaza kama ninachosikia ni cha kweli au?
Huyo aliyekuwa akisema hayo ni mwanamke na ilionekana alitoka kuelekea uani. Nikatoka ghafla, nikaona kisigino cha mguu mmoja kikimalizia kuingia chooni.
Nilirudi chumbani huku najiuliza kama hawa watu walisema vile kwa sababu wamejua mimi nimenunua bangi au? Na ni kwa nini wazungumze Kiswahili kwa mara ya kwanza siku hiyo?  
Baada ya dakika mbili, nilimsikia akirejea chumbani kwake huku akisema:
“Mimi mtu anayevuta bangi siku yoyote na mahali popote pale, nikimwona nampeleka polisi ajue mimi ni nani. Haiwezekani watu wawe wanavuta bangi hovyo tu.
Moyoni nikasema hata iweje, hii bangi leo lazima niichome humu ndani. Mkienda polisi msipoenda mtajua wenyewe. 
“Mimi siwezi kuishi katika mazingira magumu namna hii wakati pesa ni yangu. Kwa nini ustaarabu usiwepo?” nilisema moyoni nikipeleka mkono mfukoni ili kutoa ile bangi niliyonunua mara ya pili.
 Niliipata, nikaitoa. Niliiweka kwenye meza kisha nikaendelea kulala nikiusaka usingizi kwa nguvu zangu zote maana nilijisikia kuchoka sana. Hapo nilikuwa sijaenda chumbani kwangu.
Sikumbuki ni muda gani nilipitiwa na usingizi, ila nakumbuka wakati nalala ilikuwa saa kumi na moja. Nilipokuja kushtuka ilikuwa saa kumi na mbili na nusu. Ina maana nililala kwa saa moja na nusu.
Jicho langu moja kwa moja lilitua kwenye bangi pale mezani, sikuiona. 
Nilihamaki kwa kusema ha! Nani amechukua bangi yangu? Sikujibiwa na mtu, ukimya ulitawala huku akili ikiniambia wale wapangaji wenzangu watakuwa wanahusika moja kwa moja.
Baada ya muda nilitoka mle sebuleni, nikaenda chumbani. Nilifungua mlango na kusimama kwanza kabla ya kuzama ndani. Niliangaza kila kona, nikabaini kitu.
Niligundua kwamba, kuna mtu alikaa kitandani maana nilipoondoka asubuhi nilikuwa  nimekitandika, muda huo kwa pembeni upande wa mbele kulikuwa na alama za makalio.
Alama hiyo ilinipa picha kuwa, aliyekaa alikuwa na makalio makubwa sana! Nilipoangalia chini kwenye kapeti nikabini kitu kingine kwamba, aliyekaa alikuwa na mafuta kwenye miguu kwani iliweka alama kuzunguka miguu yake.
Aidha, nilibaini jambo jingine kwamba, aliyekaa kitandani pia alikuwa akisimama na kutembeatembea kwani alama ya miguu yenye mafuta ilionekana sehemu mbalimbali za chumbani kwangu.
Mara nikasikia hodi ikigongwa mlango mkubwa. Niliikumbuka ile sauti kwamba ilikuwa ya yule msukuma mkokoteni wa maji.
“Nakuja,” nilisema kwa sauti kupitia dirishani kwani chumba changu na sebule yangu vilikuwa upande wa mlango mkubwa wa kuingilia.
Nilitoka mpaka mlangoni, nikafungua na kumkuta yule kijana.
“Bro vipi, wapo wale watu ndiyo nimekuja hivi.”
Nilimshika mkono, nikamvuta kumwingiza ndani bila kusema naye. Nilimwelekeza vyumba vya wale wapangaji wenzangu kisha mimi nikaingia chumbani kwangu.
Nilikaa kitandani na kutega sikio kitakachotokea huko. Nilimsikia yule kijana akigonga mlango. Aligonga mara tatu, kisha nikasikia mlango ukifunguliwa, sikuamini. Nilitaka kutoka, lakini nikasema nisubiri hadi mwisho nione.
Baada ya mlio wa kufunguliwa kwa mlango, ukafuatia mlio wa kufungwa halafu ukapita ukimya. Akilini nilijua wamemkaribisha na wakafunga mlango na sasa wanaongea naye.
Cha ajabu, kila nilipofuatilia ili kujua kama mlango utafunguliwa na yule kijana kutoka, sikufanikiwa kugundua hali hiyo, nikaanza kupata wasiwasi.
“Inamaana tangu wakati ule hadi sasa bado wapo ndani? Wanaongea nini sasa? Au wanapigiana mahesabu? Si yule kijana alisema anadai pesa nyingi?” maswali hayo yote yalikuwa yangu lakini majibu yake sikuyajua.
Usiku uliingia, muda ukazidi kwenda, sikusikia ishara yoyote ya yule kijana kutoka. Zaidi sana nilisikia wale wapangaji wenzangu wakipika kwa kukaangiza kitu kama nyama.
Usiku nilitoka, nikaenda kutafuta chakula, nikarudi nacho nyumbani. Nikala, nikaenda kuoga, nikarudi kitandani na kulala, sikuona dalili ya mawengewenge wala mang’amng’amu.
***
Asubuhi niliamka kwa kushtuka, lakini sijui nini kilinishtua ila ni kama kuna mtu alinishika mguu. Hakukuwa na kitu chochote chumbani mwangu. Nilitoka na kwenda kusimama kwenye dirisha, nikachungulia nje. Kulikuwa shwari.
Nilipotoka kuoga nikiwa navaa nguo ili kuondoka, nikasikia wenzangu wakitoka. Nilisimama tena dirishani kwani kwa mtu anayetoka kwenye nyumba ile na kwenda popote ilikuwa lazima apite mbele ya dirisha langu.
Baada ya muda walifungua mlango mkubwa, nikasikia wakiufunga, lakini baada ya hapo sikumwona mtu yeyote yule akipita mbele ya dirisha.
Na mimi nilipomaliza kujiandaa, nilitoka, nikafungua mlango na kutoka. Mbele kidogo nilikutana na watu kama kumi wamesimama wakiongea. Niliwasalimia nikawauliza kama kuna usalama.
“Usalama ni mdogo bwana, kuna kijana mmoja amepotea. Tangu jana usiku alipotoka kwa mkewe akasema anafuatilia madeni ya biashara zake hajarudi,” alisema mzee mmoja ambaye alisimama akiwa amejishika mikono kwa nyuma.
“Ni biashara gani anafanya?” niliuliza.
“Huwa anauza maji kwenye mkokoteni.”
“Ha! Ni yule muuza maji?”
“Huyohuyo,” alisema yule mzee.
Akili za haraka nikasema hapa ndipo pa kujua wale wapangaji ni akina nani, inabidi niseme ukweli ili waende polisi, najua polisi watakuja kukagua ndani.
“Lakini mbona jana usiku alikuja kwangu kudai pesa yake?” nilihoji kwa uso wa wasiwasi.
“Ulipomlipa akaondoka?” mwanamke mmoja aliniuliza.
“Siyo kwangu, ila mimi ndiye niliyemfungulia mlango. Alipoingia akawaulizia wapangaji wenzangu, nikawaonesha chumba, akapiga hodi, akakaribishwa ndani.”
“Hukumuona kutoka?”
“Kwa kweli sikufuatilia maana na mimi nilirudi chumbani kwangu.”
Wale watu wakaniuliza kama naweza kuwapeleka pale nyumbani, nikawaambia kwa muda ule hapakuwa na mtu nyumbani, wanarudi jioni.
“Basi tunakwenda kuwaambia ndugu zake, jioni watakuja, si nyumba ile pale?”
“Ndiyo.”
Nilipofika kazini na kuanza kazi, akili zangu zikawa  zimefunguka kitu. Nilijiambia wale watu wakijua ni mimi niliyetoa mchoro wote, watanifanyaje?   
Nilibaini nimechemsha, lakini nikasema moyoni kwamba potelea mbali, wajue wasijue sawa tu.
Kuna wakati nilipigiwa simu, namba sikuitambua, yaani ilikuwa ngeni kwenye kumbukumbu zangu. Nilijiuliza mwenyewe kwamba anaweza kuwa nani, lakini sikupata jibu.
Awali nilisita kuipokea kiasi kwamba ilikata, mpigaji akapiga tena. Nikaamua kuipokea sasa:
“Halooo,” nilivuta sauti.
“Hujambo bwana?”
“Nani mwenzangu?”
“Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua nani, ungeitika kwanza kisha ndipo uniulize nani.”
“Sijambo, nani mwenzangu?”
“Angalia sana bwana,” alisema huyo mtu bila kujitambulisha kisha akataka simu.
Nilishangaa sana, nikaanza kazi ya kuwaza kwamba anaweza kuwa nani na ni kwa nini aniambie angalia sana?
“Atakuwa jamaa wa nyumbani, kwa vyovyote vile,” nilisema moyoni na kuamini hivyo kwani kwa maisha ninayoishi mimi si rahisi kuwa na maadui. Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio kwa wasiwasi. Nilijua nimeingia kwenye mapambano makubwa na wale wapangaji wenzangu.
Niliendelea kufanya kazi, lakini sikuwa na amani tena. Mara alitokea yule mfanyakazi mwenzangu ambaye alinipa ushauri wa kupulizia bangi ndani ya nyumba ili kuwakimbiza majini au viumbe wote wabaya.
“Vipi mambo yako, yamekwendaje?”
“Mambo gani?” nilimuuliza huku nikiwa namtazama. Kisa cha kumtazama kwanza ilikuwa kujiridhisha kama kweli ni yeye au wale wapangaji wenzangu wameamua kunifuata ‘laivu’.
“Si yale niliyokuelekeza kufanya.”
Nilipomkazia macho sana, akasema ana kazi nyingi, akageuza na kuondoka. Mlango ulipojifunga tu, nikajiegemeza kwenye meza na kuwaza mambo kibao. Ilikuwa kama nataka kusinzia, lakini nikasikia sauti kichwani zikisemezana hivi:
“Halooo.”
“Hujambo bwana?”
“Nani mwenzangu?”
“Hujambo, hata kusalimiana pia unataka kujua nani, ungeitika kwanza kisha ndipo uniulize nani.”
“Sijambo, nani mwenzangu?”
“Angalia sana bwana.”
Mara nikasikia tena zikisemazana hivi:
“Vipi mambo yako, yamekwendaje?”
“Mambo gani?”
“Si yale niliyokuelekeza kufanya.”
Nilishtuka na kusimama, nikaondoka kwenda nje. Nilikutana na yule mfanyakazi tena, akaniuliza kama naondoka.
“Vipi, unaondoka saa hizi?”
“Bado nipo.”
“Kwanza nilisahau kukuuliza, vipi ulifanikisha ile kitu ya kuvuta kama nilivyokwambia?”
Moyo ulishtuka, nilijua ni watu wawili kwani huyu angekuwa yule aliyenifuata muda ule, asingesema alisahau kuniuliza.
“Nilifanikiwa kupata bwana, lakini,” nilisema nikimshika mkono, nikamvutia pembeni kidogo.
“Kaka mambo makubwa kule. Kwanza unajua kama nimekuona wewe mara ya pili hii leo?”
“Kivipi?” aliniuliza.
 Nilianza kumsimulia kila kitu, kuanzia zile bangi hadi nusu saa kabla sijaonana naye. Alishangaa sana, akasema yeye ndiyo kwanza anaingia, alikuwa Kariakoo, pia akasema kwa siku hiyo ndiyo kwanza ameniona mimi muda ule.
“Sasa itakuwaje ndugu yangu?” aliniuliza.
“Sielewi.”
“Sasa sikia, mimi ninajua nitapata wapi bangi, we usiku saa moja niambie tukutane wapi, nitakuja nayo halafu  nitaiwasha na kuivuta mimi.”
“Wewe huogopi?”
“Niogope nini?”
“Kufa.”
“Nani ataniua?”
“Si hao watu wabaya.”
“Hamna, hawawezi.”
Nilimkubalia, nikamwambia nitampigia saa moja ili tukutane akiwa na hiyo bangi yake.
Akili zangu hazikukaa sawa, niliondoka kwenda kutafuta maji ya kunywa, kisha nikaenda kupumzika kwenye kibanda cha kuuza vocha za simu.
Pale, mtu yeyote anayenijua angeniona angebaini nina matatizo mazito kichwani mwangu, kwani sikuwa sawa hata usoni. Muda mwingi niliwaza maisha ya kwenye ile nyumba, hasa usiku wa siku hiyo ambapo najua wale watu wakija ndiyo balaa litakuwa kubwa zaidi.
“Halafu usiku wa leo lazima watakuja kunifanyia maajabu yao, lakini dawa yao nisilale. Oke, kumbe bangi itapulizwa leo, kidogo itakuwa nafuu,” nilisema moyoni, nikashtuliwa na sauti ya kike nyuma yangu iliyoita jina langu.
NILIPOGEUKA nyuma, nikamwona dada mmoja aitwaye Mwantumu Seleman nilikuwa naishi naye Mwananyamala. Akaniuliza habari za siku. Niliamua kumsimulia janga langu, lakini ghafla likaja gari, akaingia huku akiniambia atanitafuta siku nyingine.
Baadaye nilirudi kazini huku nikiwa na hali ya wasiwasi, hata kazi zangu zikuzifanya sawasawa kama ilivyo kawaida yangu. Iliniuma sana!
Muda wa kazi ulipokwisha, niliondoka moja kwa moja hadi nyumbani. Sikutaka kupitia mahali siku hiyo, lakini nilishakubaliana na yule mfanyakazi mwenzangu aliyesema atakuja na bangi yake.
Wakati nafungua mlango mkubwa nilibaini wenzangu walisharudi maana mlango haukufungwa na funguo, nikaingia ndani. Nilipofika kwenye mlango wangu wa kuingilia sebuleni, wakati naufungua nikasikia mlango wa chooni unafunguliwa, yaani kumaanisha kwamba kuna mtu anatoka.
Ukisimama mlangoni pangu, mtu akitoka chooni unamuona bila kificho, hususan kama anakuja vyumbani. Lakini pia hata akiwa anatoka kwenda uani, utamuona kwa mgongoni. Nilisita kuingia nikiamini nitamwona mtu huyo. Nilianza kuona miguu ikitoka, moyo wangu ukashtuka, mara nikamwona mtu mwenyewe.
Nilijikuta nikisisimka mwili, niliamini naona kivuli chake na si yeye. Ni mtu mweusi, wakati nilitarajia angekuwa mweupe.
Alivyozidi kunisogelea, nikabaini kuwa, ni yule kijana muuza maji kwenye mkokoteni.
“Ha! Wewe vipi, unatafutwa sana unajua?” nilimwambia.
Badala ya kunijibu, alikata kona kuufuata mlango mkubwa. Na mimi nikamfuata kwa nyuma, nilimkuta akiwa anamalizikia kutoka nje. Niliitupa simu kwenye kochi kisha nikatoka kumfuata, na mimi nilifungua mlango ambao ulishaanza kurudi baada ya yule kijana kutoka.
Nilishangaa kutomuona popote kule nje. Wazee wawili walikuwa wanapita, nikawauliza kama wamemuona mtu ametokea mlangoni pale, wakasema hapana, ila kuna mbwa alitokea ndani kazunguka nyumba.
“Mh! Mbwa tena?” niliwauliza wale wazee, nao wakasisitiza kuwa ni mbwa, tena mweusi.
Mapigo ya moyo yalianza kwenda mbio, wasiwasi uliongezeka kiasi cha kunifanya niishiwe nguvu. Wakati huo wale wazee walikuwa wakimalizikia kwa mbali. Niliogopa kurudi ndani, nikawa nimesimama mlangoni.
Wazo lilinijia kwamba, nimpigie simu yule mfanyakazi mwenzangu kumuomba aje mapema maana hali ni mbaya sana. Lakini simu nayo ilikuwa sebuleni kwenye kochi, nitaipataje, yaani nitaifuataje kule ndani wakati niliamini tayari kumeshakuwa ukanda wa kifo?
Niliteremka na kusimama nje kabisa, ghafla kwenye dirisha la chumbani kwangu nikaona kama mtu anachungulia nje, nilikaza macho ili kumwangalia vizuri,  akapotea.
“Mh! ni kweli?” nilijiuliza mwenyewe. Ukweli ni kwamba alikuwepo mtu, tena mweusi au niseme Mwafrika kama mimi.
Nilikwenda pale dirishani, nikapanda ili kuchungulia, nikaona mlango unafunguka kuashiria kuna mtu alitoka maana mlango ule ulikuwa hauwezi kukaa wazi, ni lazima ujifunge wenyewe na mbaya zaidi mimi nilikuwa sijaufungua zaidi ya ule wa sebuleni.
Kuna jamaa mmoja alikuwa anakuja kutokea upande ninaoondokea kwenda kazini, simfahamu lakini nilimsimamisha.
“Bro kuna ishu hapa inatisha kidogo, naomba msaada wako.”
“Kuna nini?” aliniuliza.
Nilimsimulia kila kitu cha siku ile tu lakini, sikugusia mambo ya nyuma.
“Du! Kwa hiyo mimi nikusaidieje?”
“Naomba tuingie wote ndani, nataka nikachukue simu yangu tu nimpigie huyo jamaa.”
“Da! Itakuwa ngumu kidogo, unajua mimi nina haraka sana leo,” alijitetea yule mtu ambaye kwa umbo ni bonge la mtu. Nilijua ni uoga tu, hakuwa na kuwahi wala kuchelewa.
Alipopita, akatokea mwingine, mzee mmoja, kichwa chote kilichafuka kwa mvi. Nilimsalimia huku nikimwonesha ishara kwamba nataka kuzungumza naye.
“Mzee samahani sana.”
“Bila samahani kijana.”
Naye nikamsimulia tukio la siku ile,  lakini wakati ananisikiliza, mara nilimwona anatupia macho dirishani na mimi nikageuka kuangalia, sikuona mtu.
“Umeona nini mzee wangu?”
“Nimeona msichana ananizomea.”
“Kweli?”
“Ee. Ndiyo hayo mambo unayosema?”
“Ndiyo hayo mzee.”
“Twende,” alisema, nikaanza kutangulia mbele, mzee akanifuatia kwa nyuma. Hatukuwa tukiongea chochote, najua sababu. Kila mmoja alikuwa anaiwaza hatari ya mbele.
Tuliingia ndani, tukafika sebuleni, lakini sikuiona simu kwenye kochi.
“Ona sasa mzee, simu niliitupia hapa, lakini haipo.”
“Au unayo mfukoni kijana?”
“Hapana, nina uhakika,” nilisema huku nikijipapasa mifukoni, hakukuwa na simu.
“Nitajie namba nijaribu kuibipu,” yule mzee aliniambia huku akitoa simu yake mfukoni. Nilimtajia namba zote, akawa anaziandika, kisha akapiga huku simu akiwa ameiweka kwenye sikio lake la kulia. Nilishtuka sana  kusikia simu yangu inaita kutokea kwenye chumba cha wale wapangaji wenzangu.
“Si hiyo?” yule mzee aliniambia akiniangalia kwa mshangao.
Mzee alikata kisha akapiga tena, ikaita tena kutokea kulekule, nilizidi kuogopa, nikamwambia tutoke lakini uzee kweli dawa, aliniambia hakuna haja ya kutoka dawa ni kupambana tu.
Alinisogelea na kuniambia kwa sauti ya chini:
“Niwagongee mlango?”
“Si watakasirika?”
“Sasa kama unaogopa watakasirika, unadhani simu yako utaipataje?” 
“Haya wagongee. Lakini subiri, kwa nini tusiende kwanza chumbani tukajua nani alikuwa anachungulia nje?”
“Kijana unaonekana muogamuoga sana, we mwanaume bwana, jifunze kukabiliana na hali kama hii, sawa?”
“Sawa mzee.”
“Haya twende huko chumbani kwako unakotaka tukaone huyo msichana.”
Tulifungua mlango wa chumbani, hakukuwa na mtu, ila shuka nililoliacha kitandani asubuhi silo, lilitandikwa jingine pia la kwangu.
“Khaa!” nilishangaa.
“Nini?”
“Hili shuka.”
“Limefanyaje?”
“Silo nililolitandika asubuhi.”
“Lakini la kwako?”
“Ndiyo langu.”
Niliangalia mazingira mengine ya mle ndani na kubaini kwamba, kuna vitu vingi sana vilikuwa ndivyo sivyo.
“Si umeona hayupo?” yule mzee aliniuliza, nikamjibu ndiyo, akasema twende tukachukue simu yetu kwenye kile chumba ambacho ilikuwa inaita.
Moyo wangu ulikuwa mzito sana, nilihisi kizunguzungu, nilitamani kukaa chini na kumwomba yule mzee asichukue uamuzi wa kuifuata ile simu, lakini ningeipataje simu yangu wakati ina namba kibao?
“Kijana, ngoja nikuoneshe dawa moja ya hao viumbe wasiotaka kuonekana,” alisema yule mzee, nikamuuliza ni ipi hiyo.
“Tulia wewe,” alisema huku akiingiza mkono mfukoni na kutoa kimfuko kidogo, akakifungua akatoa kitu. Nilipomuuliza ni nini akajibu:
“Ni bangi.”
“Sawa kabisa, hiyo ndiyo dawa, ngoja nikupe kiberiti.”
Katika mambo yaliyonishangaza ni hilo, tulitafuta kiberiti chumbani hadi sebuleni lakini hakikuonekana, mbaya zaidi mimi nilikuwa na kawaida ya kununua viberiti bunda zima, lakini pia sikuona popote.
“Kweli una kiberiti ndani?” yule mzee aliniuliza.
“Kiberiti kipo na uzuri ni kwamba, nina bunda zima, pia silioni.”
Nilimwona yule mzee akisimama wima na kunyoosha mikono juu kama mtu anayeomba dua kwa Mungu.
“Kijana nimejua sasa, ngoja kidogo,” alisema huku akitoka na mimi nikimfuata kwa nyuma.
Wakati tunapita kwenye korido jirani na vyumba vile vya wenzangu, nikaisikia simu yangu ikiita. 
“Mzee mzee, hiyo bwana,” nilisema, mzee akasimama na mimi nikasimama nyuma yake, tukasikia sauti ya mwanaume ikipokea simu yangu:
“Haloo…Juma…Juma gani wewe? Nakuuliza Juma gani maana mimi ndiyo mwenye simu hii, huyo unayemsema simjui na wala hajawahi kumiliki simu hii,” sauti ya kiume ilisema, ukapita ukimya kidogo kisha sauti hiyohiyo ikasema:
“Kama unabisha siyo simu yangu ongea na mke wangu huyu hapa.”
Mara nikasikia:
“Haloo…ni kwa nini mnapenda sana kumfuatafuata mume wangu, mara mzungumzie bangi, mara mtusemee kwa watu.”
Nilitamani sana kumwambia asiniache katika safari yake maana kwangu kwa muda ule palishaharibika, ningeuawa na watu wasioonekana.
“Wewe nisubiri kijana,” mzee aliniambia akiendelea kwenda nje sikukubali.
“Mzee humu ndani mimi sikai, nimeshajua sasa.”
“Umejua nini?”
“Huyo Juma anayetajwa hapo nafanya naye kazi na ilikuwa aje na bangi kwa ajili ya hawahawa watu wa humu ndani.”
Mzee aliniangalia, akaniuliza:
“Wewe kijana unaye Mungu?”
“Ninaye.”
“Huwa unakwenda kusali?”
“Sana.”
“Lini umekwenda mara ya mwisho?”
“Ungeniambia tatizo ni kusali au?”
“Si hilo tu, ila una matatizo mengi. Hivi hapa tumesimama, nyuma yako nimemuona yule msichana amekuinamia akikung’ong’a kama mara tatu kwa harakaharaka.”
Nilitimua mbio kuelekea kusikojulikana, nikaenda kufunga breki kwenye mtaa mmoja ambao ukienda kushoto kwangu unakwenda kutokea kwenye barabara ya kwenda Kigogo Mbuyuni.
Baadhi ya watu walioniona nilivyo walitambua nina tatizo zito kichwani, mzee mmoja aliniuliza kama nakimbizwa nimefumaniwa.
“Sijafumaniwa mzee, lakini kwa tatizo langu afadhali ningefumaniwa.”
Huyu mzee alikuwa amebeba kibegi kidogo mgongoni, alivaa suti nyeusi huku akionekana ni mzee mwenye heshima kubwa katika jamii inayomzunguka.
“Tatizo nini, hebu nisimulie kidogo tu,” alisema huku akinivutia pembeni. Nilimsimulia kila kitu, alichokuwa akinishangaza sasa, kila hatua ya maelezo yangu alikuwa akiachia tabasamu hata pale nilipoamini kwamba ninachokisema kwa wakati huo asingetabasamu na uso wake ungeonesha kushtuka.
Nilipomaliza nikanyamaza na kumwangalia kwa woga, nilitaka kuamini ni yule mwanaume aliyepokea simu yangu kule nyumbani amenibadilikia ili nisiweze kumtambua.
Moyoni nilisema kuwa, kama kweli ni yeye atakapojidhihirisha  tu kwangu nitoke mbio na kwenda kuingia kwenye nyumba ya mtu yeyote mbele yangu.
“Tatizo ni hilo dogo tu?” aliniuliza.
“Ni hilo tu mzee wangu. Ukiweza kunisaidia nitashukuru sana.”
“Nyumba yenyewe iko wapi?”
“Kule nyuma nyuma.”
Nilimwona akiingiza mkono mfukoni na kuchomoa simu nyeusi ndogo, wengi wanaziita za tochi kisha akabonyezabonyeza na kuiweka sikioni. Moyoni nilisema yaleyale.
“Si ajabu anawasiliana na yule mwanamke wa kule nyumbani.”
 Nikamsikia akiuliza:
“Isdory, bado mpo hapo?”
Nadhani huyo jamaa alisema yupoyupo maana nilimsikia huyo mzee akisema: “Unaweza kuja na akina Tino hapa kwenye kibanda tulichotuma pesa asubuhi ya leo? Haya njooni.”
Niligeuzageuza kichwa na kukiona kibanda cha kutuma pesa kwa kupitia mitandao mbalimbali ya simu. Nikajua amewaita watu waje pale.
Baada ya dakika kama tatu, wakafika watu kama saba, wanne wanawake, watatu wanaume akiwemo Isdory na Tino.
“Huyu bwana anaitwa,” alianza kusema yule mzee akiniangalia nikajua anataka nijitambulishe jina mimi mwenyewe, nikafanya hivyo. Nilipomaliza, ndipo yule mzee akawaambia wenzake kisa chote cha kwangu, mwanzo hadi mwisho kama nilivyomsimulia awali.
“Ndugu, sisi wote walokole, kazi hiyo tunaimudu kwa vile mara nyingi huwa tunatumia jina la Bwana na Mwokozi wetu kufukuza uchafu kama huo, sasa itabidi utupeleke kwenye hiyo nyumba,” alisema yule mzee.
Nilianza kutembea mimi na wao wakawa wananifuata kwa nyuma. Wale wanawake niliwasikia wakizungumzia mwanamke mmoja aliyeangushwa chini na mapepo akawa anataka kupigana na wale waliokuwa wakimwombea. Moyoni nikasema:
“Leo huko sijui.”
Tulifika nje ya nyumba, kitendo cha kwanza ambacho si cha kawaida, nilimwona yule kijana muuza maji akitoka ndani. Alivaa kama siku alivyokuja nikamwingiza ndani.”
Nilishtuka sana, yeye hakushtuka, ila aliponiona akaniambia:
“Bro nashukuru sana wamenilipa pesa zangu.”
Sijui ni nini kilinipata nilijikuta nikisema sawa, sikuongeza neno jingine lolote lile.
“Ni humu waheshimiwa,” niliwakaribisha wale watu nikiwa nimeshapishana na yule kijana.
Waliingia wote ndani, wakasimama katikati ya korido kisha wakawa wananiangalia, yule akaniuliza:
“Hivyo vyumba ni vipi?”
Sikumjibu kwa sauti, nilinyoosha mkono kuelekea kwenye vyumba vyote viwili. Vilioneshwa kufungwa kwa ndani lakini hakukuwa na sauti ya muziki wala maongezi yao.
“Baba katika jina la Yesu,” yule mzee alianza ghafla.
“Amiiiin,” walijibu wote aliofuatana nao, tena walijibu kwa sauti ya juu kisha wakatulia kimya. 
Akaanza kusali akitaja maneno ya kutisha, nilimsikia akisema, choma moto roho mtakatifu, mara Malaika Michael shuka na panga likatalo kuwili.
Kifupi yule mzee alisema maneno ya ki-Mungu kwa jinsi nilivyoelewa mimi. Ikafika mahali akasema:
“Paaza sauti yako.”
Ndipo wengine nao wakapokea kwa kila mmoja kuomba kivyake. Wengine walisikika wakisema wanaangusha na kuvunja ngome za ibilisi, wengine wanachoma moto makazi ya shetani, wengine wanamwagia damu ya Yesu pale ndani. Nilianza kuhisi amani iliyoje, niliamini ukombozi umefika tayari kwani sauti tu niliisikia ikipenya hadi kwenye mbavu zangu.
Waliomba sana, kuna wakati mimi nilihisi kuchoka lakini wao waliendelea tu hadi moyoni nikasema kweli ni watu wa Mungu.
Ghafla nilianza kuona moshi mweusi ukitoka chini ya milango yote ya wale ndugu, mlango wa sebuleni kama sikikosei na mlango wa chumbani. Moshi ulikuwa mzito kiasi kwamba, kuna wakati nilihisi kupaliwa na kukohoa kwa nguvu lakini wao hawakuonesha dalili ya kusumbuliwa na moshi huo.
Mara, milango yote miwili ikaanza kufunguka yenyewe polepole huku maombi yakiendelea kwa kasi na nguvu ya ajabu. Milango hiyo ilifunguka hadi ikafika mahali ndani kukaonekana.
Cha ajabu sasa, vyumba vilikuwa vyeupe, ndani yake hakukuwa na kitu chochote, hata karatasi. Ilikuwa kama chumba kilichopigwa deki au kufagiliwa kwa ajili ya maandalizi ya kuingia mkaaji mpya.
“Ha! Oneni jamani,” nilijikuta nikisema hivyo. Nilibaini kwamba, wale watu hawakuona wakati milango inafunguka kwa vile walipokuwa wakiomba walifumba macho na walikuwa wakijipigapiga kwenye viganja kwa kutumia ngumi.
Yule mzee alipoona vile akasema:

“Katika jina la Yesu.”
“Amiiin.”
“Sasa tushushe uwepo wa Bwana mahali hapa, kwamba akapafanye pawe mahali salama, penye amani na utulivu wa hali ya juu, kila mmoja sasa amwombe Bwana hivyo.” 
Wakaanza kuomba tena, safari hii si kwa kukemea kama mwanzoni, ilikuwa sauti yenye upole na utii, mara nikasikia mlango mkubwa ukigongwa kwa nguvu.
“Ngo ngo ngo ngoo.”
“Ingia,” nilisema lakini huku nikienda mlangoni, nikaufungua! Mbele yangu alisimama yule dalali.
“Karibu bwana.”
“Ee bwana nini umefanya sasa?” ndilo swali lake hata kabla ya salamu.
“Kwa nini?”
“We hujui umefanya nini? Si wako watu humo ndani, wamekuja kufanya nini hapa? Hujui kama kuna watu umewaumiza? Wewe ungefanyiwa hivyo ungekubali kweli?”   
“Kaka unajua ukija kwangu njoo kwa heshima zako zote na hoja zenye msingi, usije kama mwendawazimu mpya, wewe unachokisema mimi sijakisema kwako? Ulichukua hatua gani wakati naumia mimi?”
“Lini umeniambia?”
“Wewe sijawahi kukupigia simu kukwambia? Tena ukasema kama vipi nihame lakini sitarudishiwa kodi ya nyumba na mimi nikakujibu niko tayari kwa hilo…”
“Sasa wewe ulikuwa ukiteswa kwa lipi, weka ushahidi hapa kwamba ulikuwa ukiteseka sana.”
“Sina haja, mimi ndiyo najua.”
Wakati tukijibizana hivyo, wale waombaji walikuja juu kwa kuomba. Walipaza sauti sana wakisema moto uteketeze kila hila na jambo lolote ambalo linakwenda kinyume na mimi ndani ya nyumba ile.
Ghafla, nilimwona yule dalali akianza kuyumba kama mlenvi, alikwenda kulia, kushoto, akasimama, akawa kama ananijia mimi, nikamkwepa, akaenda kushoto na kuanguka puu!
Kwangu ilikuwa ni furaha kwani nilipata picha kwamba, yule dalali alikuwa anahusika moja kwa moja na matukio yote ya ajabu mle ndani. Niliwaita wale watu wanaofanya maombi na kuwataka washuhudie ambapo walipomwangalia dalali waliongeza mkazo wa maombi yao.
Mwisho, dalali aliamka akiwa kama hana ufahamu, alikalishwa chini na kuhojiwa ambapo alisema mambo ya ajabu sana. Alisema mwanaume aliyekuwa akiishi ndani ya vyumba vile ni yeye na mkewe, akasema mkewe ni jini kwa asilimia mia moja ila yeye si jini bali mkewe alimfanya awe na uwezo wa kutoonekana wala kujulikana na mtu.
Alipoulizwa kama alikuwa anapata faida yoyote kwa kitendo cha kugeuka kuwa jini alijibu hakuna ila alikuwa anasikia raha.
“Mfano, huyu bwana tangu ameishi humu hajawahi kutuona kwa macho lakini sisi tulikuwa tunamuona siku zote, tulikuwa tunaingia chumbani mwake na kumfanyia mambo yetu yeye hajui.”
Jambo lingine ambalo lilinishangaza sana ni pale dalali huyo aliposema yeye alikuwa na uwezo wa kujua anachokusudia kukifanya mtu hata akiwa Dodoma na akakizuia mapema. Ila, anashindwa kujua endapo mtu huyo atakuwa anakusudia kufanya jambo kwa kuliwaza moyoni mwake bila kulisema kwa mtu.
Nilimuuliza mfano, akajibu mfano ni mimi na mfanyakazi mwenzangu tulipokuwa tumepanga kutumia bangi kuwaangamizi yeye na mkewe, walijua kwa sababu tulijadili kwa sauti ndiyo maana wao walijua. Akaongeza hata nilipoingia ndani na yule mzee aliyeshindwa akatimua, walijua tumepanga ndiyo maana wakawahi kwa kuchukua simu na kufanya mahoka mengine.
Yule mzee mkubwa wa wale waombaji akamuuliza:
“Ina maana mkeo jini kwa sasa yuko wapi?”
Yule bwana akajibu atakuwa amerudi ujinini kwa sababu wakati wanaanza kuomba mkewe ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhisi anaungua moto na kuanza kulia kwa sauti mpaka ndugu zake wakajitokeza kumtwaa kwenda naye ujinini.
Yule mzee mkubwa wao akauliza swali jingine ambalo na mimi nilitaka kuuliza. Alimuuliza hivi:
“Sasa watu wanasema majini wana uwezo mkubwa, wanaweza kupata fedha na mali yoyote ile, sasa kama wewe ulikuwa mume wa jini kweli ni kwa nini aliamua uwe dalali?”
Dalali akajibu: “Mimi sikuwa dalali, bali nilijifanya dalali ili nipate mtu wa kumpangisha ndani kwa sababu mimi na mke wangu tulipenda kuwachezea watu wanaoishi ndani.
“Mimi nina eneo Ilala la kuuza magari, pia nina duka kubwa sana Mnazi Mmoja, sina shida ya maisha wala ya fedha.”
Kwa maneno yake hayo nilikubaliana na yeye kwani ni kweli hali yake haikuwa ya kuchoka. Hata siku ya kwanza nilipokutana naye nilishangaa dalali gani ana mwonekano wa kibosibosi ingawa hakuwa na gari. Hapo na mimi nikapata nguvu ya kumuuliza swali:
“Sasa bwana dalali wa bandia, uliwezaje kusababisha mimi nipate namba yako ya simu kwa rafiki yangu anaitwa Mohamed Kombe na akasema wewe ni dalali unaitwa Yusuf Mwamba?”
“Sikia bwana Humuli. Nimeshasema sisi tuna uwezo wa kujua kile kinachojadiliwa mahali na kukifanyia kazi. Dalali anayeitwa Yusuf Mwamba yupo, huyo rafiki yako tulimchezesha ulimi wakati wa kutaja namba, akazitaja zangu badala ya za Yusuf.”
Nilichoka kabisa, yule mzee mkuu akasema tumwingize ndani maana watu waliokuwa wakipita walianza kukodolea macho pale nje.
Kule ndani, dalali aliendelea kuzungumza mambo mengi sana lakini kuna wakati alijipinda na kujishika mgongo akidai anahisi maumivu makali ya moto. Alisema sehemu hiyo ipo kama kuna mtu amebandika jiko la mkaa.
“Mungu amekuponya sana labda kama hutajutia matendo yako ya nyuma,” alisema yule mzee aliyenisaidia.
“Mimi sitaki tena, kwanza najuta kwa nini niligeuka adui na kufanya vile kwa watu wengine. Naomba mniombee sana kwa huyo Mungu wetu.”
Yule mzee alimwelekeza kanisa lake ambalo halikuwa mbali na pale nyumbani, yule dalali akasema atakwenda kesho yake mapema.
Mimi pia nilialikwa, nikakubali kwenda kesho yake. Walipoondoka, nilibaki na dalali. Wasiwasi ulinishika lakini nikawa nasikilizia. Kila baada ya dakika tano dalali aliingia chumbani kwangu na kuniomba nimsamehe kwa yote yaliyopita.
Usiku nililala usingizi mzuri hadi kunakucha kiasi kwamba sikuamini kama ni kweli ile nyumba ilikuwa vile. Kesho yake nilikwenda kazini, jioni nilikwenda kwenye lile kanisa ambapo nilimkuta dalali ameshafika.
Tulianza kuwa waumini wa kanisa hilo. Baada ya wiki mbili, dalali alimleta mke wake  na mtoto mmoja ndani, kumbe alioa na familia yake ilikuwa Dodoma. Baada ya mwezi mmoja na mimi nilihamia Buguruni ambapo nilioa lakini bado nasali kulekule Magomeni na yule dalali.
Namshukuru sana Mungu kwa kunipigania. Ile mikono ilikuwa si salama bila neema ya Mungu. Nadhani shetani alipanga nife lakini ameshindwa katika jina la Yesu. Amina.
                                                    MWISHO.
                                                    THE END 

1 comment:

  1. Jina langu ni Lilian N.Hii ni siku ya furaha sana ya maisha yangu kwa sababu ya msaada wa Dragaguru amenipatia kwa kunisaidia kupata mume wangu wa zamani na uchawi na kupenda. Nilikuwa nimeolewa kwa miaka 6 na ilikuwa ni ya kutisha sana kwa sababu mume wangu alikuwa anajaribu kudanganya juu yangu na alikuwa akitafuta talaka lakini nilipoona barua pepe ya Dr.saguru kwenye mtandao juu ya jinsi amewasaidia watu wengi kupata zamani yao na kusaidia kurekebisha uhusiano. na kuwafanya watu wawe na furaha katika uhusiano wao. Nilimfafanua hali yangu na kisha nikitafuta msaada wake lakini kwa kushangaza kwangu zaidi, aliniambia kwamba ataniunga mkono na kesi yangu na hapa ninaadhimisha sasa kwa sababu Mume wangu amebadilisha kabisa kwa mema. Daima anataka kuwa na mimi na hawezi kufanya chochote bila ya sasa. Ninafurahia sana ndoa yangu, ni sherehe kubwa. Nitaendelea kutoa ushuhuda kwenye mtandao kwa sababu Dragaguru ni kweli harufu halisi ya spell. Je, unahitaji kupasa kuwasiliana na mkurugenzi SAGURU sasa VIA EMAIL: drsagurusolutions@gmail.com au Whatsapp +2349037545183 Yeye ndiye jibu pekee kwa tatizo lako na hufanya uwe na furaha katika uhusiano wako.
    1 wapenzi SPELL
    2 WIN EX BACK
    3 FRUIT YA WOMB
    4 PROMOTION SPELL
    5 SPOTE YA KUJIBU
    6 BUSINESS SPELL
    7 JODA YA KIENDA
    8 LOTTERY SPELL na COURT CASE SPELL.

    ReplyDelete